Prof. Lipumba ashinda kwa kishindo Uenyekiti CUF, hatma ya Maalim Seif ipo mikononi mwake

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahm Lipumba amefanikiwa kutetea nafasi yake hiyo kwa mara ya tano, baada ya kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika jana, ambapo alikabiliwa na washindani wengine wawili.

Related image
Prof. Lipumba

Washindani waliojitokeza dhidi yake ni pamoja na Mwenyekiti Wanawake wa CUF tawi la Ubungo jijini Dar es Salaam, Diana Daudi Simba na aliyekuwa mgombea wa Ubunge jimbo la Arusha Mjini mwaka 2015 kwa tiketi ya CUF ambaye pia ni Katibu wa CUF mkoani Arusha, Zuberi Mwinyi Hamisi.

Katika uchaguzi huo wa mwaka 2015 huko Arusha, Zuberi alipata kura 106, wakati mshindi alikuwa Godbless Lema wa Chadema aliyepata kura 68,868. Katika uchaguzi wa jana, Lipumba alichaguliwa kwa kura 516 sawa na asilimia 88.9, Zuberi alipata kura 36 sawa na asilimia 6.2 huku Diana akipata kura 16 ambazo ni sawa na asilimia 2.8. Kura za jumla zilizopigwa ni 598.

Kwa ushindi huo wa kishindo, Prof. Lipumba atakiongoza tena chama hicho kwa miaka mingine mitano huku leo akitarajiwa kutaja jina la atakayekuwa Katibu Mkuu wa CUF.

Hatua hiyo inatokana na mabadiliko ya katiba ya chama hicho, yanayompatia madaraka mwenyekiti wa CUF kuchagua katibu mkuu, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo alikuwa akichaguliwa na mkutano mkuu wa chama.

Mabadiliko hayo yaliyofanywa na mkutano huo, yamefuta utaratibu wa awali ambao katibu mkuu alikuwa akichaguliwa na mkutano mkuu na sasa Profesa Lipumba atakuwa ameshikilia hatima ya Maalim Seif.

Kabla ya kutangazwa matokeo ya nafasi ya mwenyekiti, yalianza kutangazwa matokeo ya makamu mwenyekiti wa CUF Zanzibar na kisha CUF Bara. Kwa upande wa CUF Zanzibar aliyeibuka mshindi ni Abbas Juma Muhunzi aliyepata kura 349 ambazo ni sawa na asilimia 60.9. Nafasi ya pili ilishikwa na Ally Rashid Abaran aliyepata kura 131 sawa na asilimia 22.7, Mohamed Habib Mnyaa alipata kura 78 ambazo ni sawa na asilimia 13.5 na Mbaruk Seif Salum alipata kura nne sawa na asilimia 0.7.

Kwa upande wake Tanzania Bara, Maftah Nachuma aliibuka kidedea kwa kupata kura 231 sawa na kura 40.9 akifuatiwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Lindi, Salum Baruan ambaye alijiunga kwenye kundi la CUF Lipumba juzi kwenye mkutano mkuu na kujaza fomu ya kuomba uongozi juzi hiyo.

Baruan alipata kura 151, sawa na asilimia 23.6. Aliyeshika nafasi ya tatu ni Abeid Ally aliyepata kura 135 sawa na asilimia 20.4, Amir Bahat Abdalla kura 14 sawa na asilimia 2.5, Severin Magese kura 13 sawa na asilimia 2.3 na Aboud Omary alipata kura 11 sawa na silimia 1.9.

Baada ya kutangazwa mshindi, Profesa Lipumba aliwataka wanachama wa CUF kujipanga kwa kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa, utakaofanyika baadaye mwaka huu. Aliwataka pia kujipanga kwa ushindi kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwakani.

Tunachotakiwa ni kuhakikisha kuwa kila uchaguzi unaokuja mbele yetu ni tunashinda kwa kila namna, iwe ni Bara au Zanzibar, na lengo kubwa ni kuwa na serikali bora itakayoundwa na CUF ya Umoja wa Kitaifa, sisi ni washindi na kilichobakia kwa sasa ni kuonesha uwezo wetu na kesho(leo) tutamjua Katibu Mkuu wa CUF na fitina zote kwisha”.

Chanzo: Habari Leo

The post Prof. Lipumba ashinda kwa kishindo Uenyekiti CUF, hatma ya Maalim Seif ipo mikononi mwake appeared first on Bongo5.com.

Pin It

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *