Bobi Wine akamatwa, tamasha lake la muziki lapigwa ‘STOP’

Mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi jina maarufu Bobi Wine amekamatwa baada ya yeye na wafuasi wake kugombana na maafisa wa polisi kufuatia hatua ya mamlaka kufutilia mbali tamasha lake la muziki la siku kuu ya pasaka.

Hali ya wasiwasi ilitanda baada ya maafisa wa polisi kuuzuia msafara uliokuwa ukiongozwa na mbunge huyo katika tamasha lake la One Love huko Busabala.

Kulingana na gazeti la Daily Monitor nchini Uganda Mbunge wa Makindye Magharibi Allan Ssewanyana alizirai na ikalazimika wafuasi wake kumbeba hadi katika gari moja ambalo lilikuwa likimsubiri.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Waandalizi wa tamasha hilo nao pia wanadaiwa kukamatwa .

Wawili hao walikamatwa mapema siku ya Jumatatu na kuzuiliwa katika gari moja la maafisa wa polisi kabla gari hilo kuondoka nao.

Kukamatwa kwa Bobi Wine kunajiri baada ya Rais Yoweri Museveni kusema kuwa hatokubali matamasha ya muziki uliojaa siasa na kuonya kwamba katika siku za usoni hakuna mtu atakayefidiwa kwa matamasha ambayo yamefutiliwa mbali kutokana na siasa.

Rais huyo alitoa onyo hilo wakati wa mkutano na wanachama na mapromota wa muziki nchini Uganda pamoja na wamiliki wa maeneo yanaopigwa muziki huo katika Ikulu ambapo alitoa shilingi bilioni mbili za Uganda kama fidia ya hasara waliopata baada ya maafisa wa polisi kufutilia mbali matamasha ya muziki wa Bobi Wine.

Bobi Wine alikamatwa na kuingizwa katika gari la polisi na kupelekwa eneo lisilojulikana.

Awali polisi walitumia nguvu kulifungua gari ambalo mbunge huyo alikuwa akiabiri kabla ya kuvunja vioo vyake na kumtoa nje.

Hatahivyo mwanamuziki Nubian Li ambaye alikuwa akiandamana naye katika gari hilo hakukamatwa.

The post Bobi Wine akamatwa, tamasha lake la muziki lapigwa ‘STOP’ appeared first on Bongo5.com.

Pin It

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *